LONDON, Uingereza – Kwa mara ya kwanza, serikali ya Uingereza imefanya operesheni ya kuizuia meli ya mafuta inayohusishwa na kile kinachoitwa “msafara wa kivuli” (shadow fleet) wa Urusi, tukio ambalo limeacha mwangwi mkubwa katika anga za kimataifa.
Operesheni hiyo ya kushtukiza imetokea alfajiri ya leo katika mkondo wa bahari wa English Channel, kufuatia amri ya moja kwa moja iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza, Keir Starmer. Meli hiyo ilikuwa ikijaribu kupita katika eneo hilo la kimkakati kabla ya kunaswa na vikosi vya usalama vya Uingereza.
Akizungumza kwa njia ya taarifa rasmi aliyoandika kwenye ukurasa wake wa X, Waziri Mkuu Starmer amesema kuwa hatua hiyo ni pigo lingine nzito kwa Urusi na ni onyo kwa wote wanaofadhili vita vya Rais Vladimir Putin nchini Ukraine.
“Operesheni hii iliyofanikiwa inatoa pigo jingine kwa Urusi na inawakumbusha wale wanaochochea vita vya Putin nchini Ukraine kwamba hatutawaruhusu wajifiche,” alisema Starmer kupitia ujumbe wake.
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa shukrani za dhati kwa Jeshi la Uingereza na maofisa wa usalama kwa utendaji wao uliotukuka, akisisitiza kuwa wanafanya kazi usiku na mchana, siku 365 kwa mwaka ili kuhakikisha nchi hiyo inabaki salama.
Tukio hili linaashiria kuongezeka kwa shinikizo la nchi za Magharibi dhidi ya miundombinu ya usafirishaji wa mafuta ya Urusi.