PARIS – Kampuni ya utengenezaji wa ndege ya Dassault Aviation imetangaza nia yake ya kudai fidia kutoka kwa Airbus, kufuatia hatua ya Ufaransa kusitisha mpango wa ununuzi wa ndege zisizo na rubani za Eurodrone, mradi wenye thamani ya Euro bilioni 7.

Kulingana na ripoti ya shirika la habari la Reuters, uamuzi huo wa Ufaransa umeathiri moja kwa moja mfumo wa “geo-return” wa programu hiyo, hali iliyopunguza kiwango cha kazi ambacho makampuni ya Ufaransa yalitarajiwa kufanya katika mradi huo.

Ingawa serikali ya Ufaransa haijajiondoa rasmi katika mradi huo wa Eurodrone, bajeti ya hivi karibuni ya ulinzi imeondoa kabisa ufadhili wa ununuzi wa ndege hizo hadi kufikia mwaka 2035. Maafisa wa ulinzi wameeleza kuwa uamuzi huo umetokana na upatikanaji wa njia mbadala za bei nafuu, ambazo zinaonekana kuendana zaidi na mahitaji ya vita vya kisasa vya kiwango cha juu.

Akijibu hatua hiyo, msemaji wa Dassault amesisitiza kuwa kampuni hiyo inapaswa kufidiwa kwa uwekezaji iliofanya katika mradi huo, ambao sasa umeathiriwa na mabadiliko ya ghafla ya manunuzi.

Kwa upande mwingine, Airbus imetoa taarifa ikibainisha kuwa ina imani mradi wa Eurodrone utaendelea kama ulivyopangwa, ingawa sasa utafanyiwa marekebisho ya kimfumo ili kukabiliana na changamoto za sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *