WASHINGTON, MAREKANI
Rais wa Marekani, Donald Trump, amedai kuwepo kwa taifa la Israel kunategemea mchango wake binafsi, huku akionyesha kutoridhishwa na namna nchi hiyo inavyoendesha operesheni zake za kijeshi nchini Lebanon.
Katika mfululizo wa matamshi yake ya hivi karibuni, Rais Trump amesisitiza kuwa bila jitihada na ulinzi wake, taifa la Israel lisingekuwa na uwezo wa kuendelea kuwepo duniani. “Bila mimi, hakutakuwa na Israel,” alikaririwa kiongozi huyo.
Aidha, Rais Trump amefichua kuwa amewasilisha ujumbe kwa serikali ya Israel akieleza kuwa haungi mkono mashambulizi yanayofanywa na jeshi la nchi hiyo katika mji wa Beirut, Lebanon. Trump amebainisha kuwa amechukizwa na namna Israel inavyoshughulikia mgogoro wa Lebanon, akisema kuwa hali hiyo hairidhishi.
Katika kile kinachoonekana kama shinikizo la wazi kwa uongozi wa Israel, Rais Trump amemtaka Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu kuongeza umakini na kuwa na uwajibikaji mkubwa zaidi kuhusiana na hatua zinazochukuliwa dhidi ya Lebanon.
“Sijafurahishwa na jinsi Israel inavyoshughulika na Lebanon. Netanyahu lazima sasa awe na uwajibikaji zaidi,” aliongeza Rais Trump.
Kauli hizi za Rais Trump zinakuja wakati ambapo hali ya usalama Mashariki ya Kati ikiendelea kuwa tete, huku kiongozi huyo akisisitiza msimamo wake juu ya hatma ya kanda hiyo na ushirika kati ya Marekani na Israel.