MINSK, BELARUS
Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko, ametoa tamko zito na la kulaani vikali hatua za kijeshi zinazochukuliwa na Israel katika Ukanda wa Gaza, akihoji uhalali wa mashambulizi hayo dhidi ya raia wasio na hatia.
Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji mkali zaidi kutoka kwake tangu kuanza kwa mzozo huo, Rais Lukashenko ameitaka serikali ya Israel kurejea katika hali ya kawaida na kutafakari upya mustakabali wake.
Hoja Kuhusu Mauaji na Historia
Akizungumzia kadhia hiyo, Lukashenko amepuuzia hoja ya kutumia historia ya ‘Holocaust’ (maangamizi makuu ya Wayahudi) kama ngao ya kutekeleza mauaji ya sasa.
“Ni tukio gani la Holocaust ambalo Waisrael wanalizungumzia, linaloweza kuhalalisha mauaji ya watu wengi kiasi hiki, hasa wanawake na watoto?” alihoji Lukashenko kwa mshangao.
Aliongeza kuwa idadi kubwa ya watoto wamepoteza maisha Gaza na kwamba jeshi la Israel limefuta kila kitu katika uso wa dunia ndani ya eneo hilo.
Upumbavu Mtupu
Rais huyo pia amekemea vikali kile alichokiita kuwa ni mipango ya “ajabu” inayodaiwa kupangwa na baadhi ya watu nchini Israel. Lukashenko ameshutumu taarifa za kuwepo kwa nia ya kujenga maeneo ya mapumziko na starehe (resorts) juu ya maeneo yaliyoharibiwa ambayo bado yana miili ya watu.
“Sasa wanazungumzia kujenga aina fulani ya maeneo ya starehe juu ya mifupa ya wafu. Huo ni upumbavu mtupu,” alisema Rais Lukashenko.
Onyo kwa Israel
Katika hitimisho la kauli yake, kiongozi huyo wa Belarus ametoa onyo akisema kuwa ni wakati muafaka kwa Israel kuzinduka na kutathmini kwa kina namna mataifa mengine yanavyoichukulia na jinsi itakavyoweza kuendelea kuwepo hapo baadaye.
“Israel inahitaji kurejea katika fahamu zake na kutafakari juu ya kuwepo kwake hapo baadaye,” alisisitiza kiongozi huyo.
Kauli hii ya Lukashenko inakuja wakati shinikizo la kimataifa likizidi kuongezeka dhidi ya Israel kutokana na hali mbaya ya kibinadamu inayoshuhudiwa katika Ukanda wa Gaza.