Marekani – Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limeibua mjadala mzito baada ya kupendekeza mechi ya ufunguzi ya tamasha lake la kwanza la soka la vijana wenye umri chini ya miaka 15 (U-15) liwe kati ya timu za Israel na Palestina.
Mashindano haya mapya, yaliyopangwa kufanyika nchini Marekani mwezi Septemba, yanalenga kuwakutanisha vijana kutoka mataifa 211 wanachama wa FIFA. Hatua hii imetafsiriwa na baadhi kama jaribio lingine la Rais wa FIFA, Gianni Infantino, kutumia soka kama nyenzo ya kukuza amani na upatanisho.
Juhudi hizi zinakuja kufuatia jaribio la awali la Infantino mwezi Aprili katika kongamano la FIFA, ambapo alijaribu kuwaunganisha viongozi wa vyama vya soka vya pande zote mbili kwa ajili ya kupeana mikono, hatua ambayo haikufanikiwa.
Baadhi wametaja suala hili kama jaribio la FIFA kusafisha maovu ya Israel, haswa ikizingatiwa kushindwa kwa FIFA kuipiga marufuku Israel. Shirikisho hilo halikuona haya kusema kwamba soka haitotumika kutatua matatizo ya kisiasa ikisahau marufuku yake kwa Urusi.
Ingawa Shirikisho la Soka la utawala wa Kizayuni wa Israel limeonyesha utayari wa kushiriki kwa ajili ya kukuza amani, upande wa Palestina bado haujatoa tamko rasmi. Dunia inasubiri kuona iwapo mashindano haya yatakuwa chachu ya umoja au changamoto nyingine ya kidiplomasia uwanjani.