VIENNA, AUSTRIA – Shinikizo dhidi ya viongozi wenye msimamo mkali nchini Israel limezidi kupamba moto barani Ulaya baada ya nchi ya Austria kutangaza kuunga mkono pendekezo la kupigwa marufuku kwa Waziri wa Usalama wa Taifa wa nchi hiyo, Itamar Ben-Gvir, kuingia barani humo.
Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa na gazeti la Kronen Zeitung, idadi ya wanasiasa mashuhuri ndani ya Umoja wa Ulaya (EU) wanaotaka kuwekewa vikwazo kwa wajumbe wa baraza la mawaziri la utawala wa Israel imeendelea kuongezeka. Hatua hiyo inakuja kutokana na mfululizo wa ghasia na ukandamizaji unaofanywa dhidi ya Wapalestina katika eneo la Ukingo wa Magharibi (West Bank).
Katika msimamo mkali zaidi, mwanasiasa mashuhuri wa Austria, Beate Meinl-Reisinger, amejitokeza waziwazi kupinga vitendo vya Waziri Ben-Gvir, ambaye anajulikana kwa sera zake kali za mrengo wa kulia.
Akizungumza siku ya Jumatatu pambezoni mwa mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Ulaya uliofanyika mjini Luxembourg, Meinl-Reisinger alibainisha kuwa mienendo ya waziri huyo haikubaliki. Alisisitiza kuwa msimamo huo unatokana na dharau na tabia za kikatili ambazo Ben-Gvir amekuwa akizionesha, hususan dhidi ya wahudumu na washiriki wa misafara ya kutoa misaada ya kibinadamu kuelekea Ukanda wa Gaza.
“Mtu huyu hakaribishwi hapa kwetu,” alikaririwa Meinl-Reisinger, akionyesha msisitizo wa Austria katika kuungana na mataifa mengine wanachama wa EU yanayotaka kuwajibishwa kwa viongozi wanaochochea uvunjifu wa haki za binadamu.
Hatua hii ya Austria inatajwa kuwa pigo kadiplomasia kwa serikali ya Israel, ikizingatiwa kuwa mataifa mengi ya Ulaya sasa yanaanza kuchukua hatua madhubuti za kivitendo badala ya kutoa matamko ya kulaani pekee.