AWASHINGTON – Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, amezua taharuki katika duru za kisiasa baada ya kutoa kauli inayopingana na Rais Donald Trump kuhusu operesheni za mafuta nchini Iran.

Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge siku ya Jumatano, Wright alieleza bayana kuwa hana taarifa zozote zinazothibitisha kuwa Marekani imechukua mamilioni ya mapipa ya mafuta kutoka Iran. Kauli hiyo imekuja kufuatia madai yaliyotolewa hivi karibuni na Rais Donald Trump, ambaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa Marekani imefanikiwa kutaifisha kiasi kikubwa cha mafuta hayo.

Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kama ufafanuzi wa kiufundi, Waziri Wright alikiri kuwa jeshi la Marekani limekuwa likitoa msaada wa kiusalama ili kuwezesha usafirishaji wa mafuta kupitia Mlango-bahari wa Hormuz (Strait of Hormuz). Eneo hilo ni njia muhimu na nyeti ya maji inayotenganisha nchi za Iran na Oman, ambayo hutumiwa na meli nyingi za mafuta duniani.

Aidha, Wright aliongeza kuwa harakati za usafirishaji wa mafuta katika mlango-bahari huo zimeongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi cha wiki moja iliyopita. Ongezeko hilo linatajwa kuwa la “maana sana,” jambo linaloashiria kuimarika kwa shughuli za kibiashara na usafirishaji katika eneo hilo licha ya mivutano ya kisiasa.

Mkanganyiko huu wa kauli kati ya Waziri huyo na Rais Trump umezua maswali miongoni mwa wabunge kuhusu usahihi wa taarifa za operesheni za Marekani katika Mashariki ya Kati, huku macho ya wadau wa nishati duniani yakiendelea kutumbulia kile kinachoendelea katika Mlango-bahari wa Hormuz.

Leave a Reply