PARIS, UFARANSA
Ufaransa na Ujerumani zimeshindwa kuvunja ukuta wa kutoelewana uliodumu kwa miezi kadhaa kuhusu mradi wao wa pamoja wa kutengeneza ndege za kivita za kisasa (Next-Generation Fighter Jet), hatua inayozua maswali juu ya hatima ya ushirikiano huo wa kijeshi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Ufaransa (Élysée) siku ya Jumatatu, kushindikana kwa makubaliano hayo kumekuja baada ya majadiliano ya kina yaliyofanyika wiki iliyopita kati ya Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, na Kansela wa Ujerumani, Friedrich Merz.
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, baada ya tathmini ya viongozi hao, pande zote mbili zimefikia hitimisho kuwa makampuni ya ulinzi yanayohusika na mradi huo hayawezi kupiga hatua zaidi kutokana na kutofautiana kwa mitazamo na maslahi ya kiufundi.
Aidha, Ikulu ya Élysée imeongeza kuwa mamlaka nchini Ujerumani zimeeleza kuwa haziwezi tena kuendelea kuyashinikiza makampuni hayo ya ulinzi kufikia mwafaka, jambo ambalo limekwamisha mchakato huo uliokuwa ukisubiriwa kwa hamu kuimarisha ulinzi wa Ulaya.
Kukwama kwa mradi huu kunatajwa kuwa pigo kwa jitihada za nchi hizo mbili zenye nguvu barani Ulaya katika kuunganisha nguvu za kijeshi na teknolojia ya kisasa ya anga.