Katika hali ya kushangaza na inayoashiria kubadilika kwa upepo wa kisiasa, Rais wa Marekani ametangaza kusitisha mpango wa mashambulizi ya kijeshi uliokuwa umepangwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran usiku wa leo. Trump kwa mara nyengine amedai kuwa uamuzi huo umekuja baada ya mazungumzo ya kidiplomasia kufikia ngazi ya juu kabisa ya uongozi nchini Iran.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Rais Trump amebainisha kuwa ametoa amri ya kufuta mashambulizi na ulipuaji wa mabomu uliopangwa kufanyika usiku wa leo. Kwa mujibu wa kiongozi huyo, hatua hiyo inafuatia kile alichokiita “uthibitisho wa makubaliano” kutoka kwa viongozi wakuu wa Tehran.
Inadaiwa kuwa maelezo ya kina ya makubaliano hayo yamejadiliwa na kupitishwa na pande zote zinazohusika. Trump ameorodhesha mataifa kadhaa yaliyohusika katika mchakato huo, ikiwemo Israel, Saudi Arabia, Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Uturuki, Pakistan, Bahrain, Kuwait, Jordan, na Misri.
Hata hivyo, Rais huyo amesisitiza kuwa mzingiro wa kijeshi baharini (naval blockade) utaendelea kudumishwa kama shinikizo hadi hapo makubaliano hayo yatakapokamilika rasmi. Amesema kuwa muda na mahali pa utiaji saini wa mkataba huo vitatangazwa hivi karibuni.
Licha ya madai hayo mazito ya Trump, viongozi wa Iran mpaka sasa wamekaa kimya na hawajatoa tamko lolote rasmi. Wachambuzi wa mambo wanaangazia kwa mashaka kauli hizi, wakikumbusha kuwa tangu kuanza kwa mzozo huu, Trump amekuwa akitoa mfululizo wa kauli zinazopingana na ambazo mara nyingi zimeonekana kutoendana na uhalisia wa mambo nyanjani.