TEHRAN, IRAN – Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetoa tamko zito kuhusu mwelekeo wa amani katika ukanda wa Mashariki ya Kati, ikisisitiza kuwa kukomeshwa kwa vita nchini Lebanon ni sharti lisiloweza kutenganishwa na makubaliano yoyote ya jumla ya kusitisha mapigano.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, amebainisha kuwa nchi hiyo inafuatilia kwa umakini mkubwa utekelezaji wa ahadi na majukumu ya kimataifa kutoka kwa pande zinazopingana. Baghaei alifichua kuwa, wakati mchakato wa makubaliano ukiwa katika hatua za lala-salama, utawala wa Israel ulifanya shambulio la kigaidi kwenye makazi ya watu nchini Lebanon, lililosababisha kifo cha kamanda mkuu wa Hezbollah na raia wasio na hatia.
Diplomasia Katikati ya Mashambulizi
Licha ya kile alichokiita “uovu wa Israel” wenye lengo la kuvuruga juhudi za amani, msemaji huyo alieleza kuwa Iran imedumisha umakini wake katika diplomasia. Amesema kuwa shambulio hilo halikufanikiwa kuondoa mwelekeo wa kimkakati wa Iran, bali limegeuka kuwa fursa ya kuimarisha na kuunganisha zaidi “Mhimili wa Upinzani” (Resistance Front).
Makubaliano ya Jumla
Baghaei alisisitiza kuwa kusitishwa kwa mapigano na kukomesha vita nchini Lebanon ni sehemu ya msingi ya makubaliano mapana ya amani yaliyopitishwa tangu tarehe 7 Aprili (19 Farvardin). Aliongeza kuwa msimamo wa Iran ni kuhakikisha kuwa Lebanon inapata utulivu wa kudumu kama sehemu ya suluhu ya kikanda.
Onyo kwa Pande Husika
Akihitimisha tamko lake, Baghaei amesema Iran imethibitisha nia yake ya dhati na itaendelea kufuatilia mabadiliko yoyote yajayo kwa umakini wa hali ya juu. Amesema kuwa Tehran haitasita kutumia “zana zake zote za kimkakati” ili kuhakikisha kuwa upande wa pili unatekeleza ahadi zake kikamilifu na kuzuia ukiukwaji wa makubaliano hayo.