Seneta wa Marekani, Jon Ossoff, ametoa shutuma nzito dhidi ya utawala wa Donald Trump, akiutaja mzozo wa kivita na nchi ya Iran kama pigo kubwa na “janga” kwa sera za kigeni, uchumi, na usalama wa taifa la Marekani.
Akizungumza kwa hisia kali, Seneta Ossoff amebainisha kuwa tangu siku ya kwanza ya mzozo huo, Rais Trump aliupotosha umma kwa kutoa uhakika usio na msingi kuwa operesheni hiyo ilikuwa ikienda kwa kasi zaidi ya ilivyopangwa. Ossoff amedai kuwa rais huyo aliendeleza mlolongo wa kauli za uongo, akijitangazia ushindi kila uchao, huku akidai kuwa mafanikio yalikuwa karibu, wakati hali halisi ilikuwa tofauti.
“Huu ni udhalilishaji mkubwa unaotokana na kufeli kwa sera zake za kigeni katika ukanda wa Mashariki ya Kati,” alisema Seneta Ossoff. Aliongeza kuwa hatua hizo zimeiacha Marekani katika hali ya hatari zaidi kuliko hapo awali, huku zikiteketeza mabilioni ya dola za walipa kodi.
Aidha, Seneta huyo ameeleza kusikitishwa kwake na upotevu mkubwa wa zana na vifaa vya kijeshi vilivyotumika kwenye mzozo huo, akisisitiza kuwa itachukua miaka mingi kwa jeshi la Marekani kufidia pengo hilo la kijeshi.
Akihitimisha hoja yake, Ossoff amesema kuwa hadhi ya Marekani katika jukwaa la kimataifa imeshuka kwa kiasi kikubwa. Amesema kuwa taifa hilo sasa linakabiliwa na kibarua kigumu cha kujijenga upya kutokana na kile alichokiita “mwanguko wa sera za nje” chini ya uongozi wa Trump, mchakato ambao amekiri kuwa utachukua miaka mingi kukamilika.