ROMA, ITALIA – Hali ya kidiplomasia kati ya Marekani na Italia imeingia katika msukosuko mkubwa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutoa kauli za kudhalilisha dhidi ya Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, jambo lililopelekea nchi hiyo kufuta safari rasmi za kiserikali kuelekea nchini Marekani.

Mzozo huo uliibuka baada ya Trump, akizungumza na kituo kimoja cha televisheni nchini Italia, kudai kuwa Bi. Meloni “alimbembeleza kwa machozi” ili wapige picha pamoja wakati wa mkutano wa kilele wa G7 uliofanyika Évian. Trump alikwenda mbali zaidi na kusema kuwa alihisi “kumhurumia” kiongozi huyo, akiongeza kuwa hakuwa hata na “wajibu” wa kuzungumza naye.

Meloni Ajibu Mapigo
Akijibu shutuma hizo kupitia ujumbe wa video, Waziri Mkuu Giorgia Meloni ameonekana kughadhibishwa na kauli hizo, akizitaja kuwa ni “uongo wa kutengenezwa.” Meloni amesema amepigwa na butwaa na kusema kwa msisitizo: “Mimi na Italia hatujawahi na hatutawahi kubembeleza mtu yeyote.”

Hatua za Kidiplomasia
Kufuatia matamshi hayo yanayoonekana kama dharau kwa taifa la Italia, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Antonio Tajani, amechukua hatua ya haraka kwa kufuta safari yake ya kikazi iliyokuwa imepangwa kuelekea Miami, nchini Marekani.

Waziri Tajani amezitaja kauli za Trump kuwa ni “nzito na za kashfa” si tu kwa kiongozi wa nchi, bali kwa heshima ya taifa zima la Italia.

Mvutano huu unakuja wakati ambapo mahusiano kati ya mataifa hayo mawili washirika wa kihistoria yameingia kwenye mtihani, huku wachambuzi wa mambo wakisubiri kuona namna hali hiyo itakavyotatuliwa katika anga za kidiplomasia.

Leave a Reply