TEHRAN, IRAN – Katika hali ya kuongezeka kwa mvutano katika Mashariki ya Kati, jeshi la Iran kupitia makao makuu yake ya Khatam al-Anbia, limetangaza rasmi kufungwa kwa Mlango-Bahari wa Hormuz kwa usafiri wote wa meli.

Katika taarifa iliyotolewa mapema leo, jeshi la Iran limetaja sababu za kuchukua hatua hiyo nzito kuwa ni kile walichokiita ni ukiukwaji wa mkataba wa maelewano (MOU) uliolenga kumaliza vita, ukiukwaji ambao Iran inailaumu Marekani. Aidha, Tehran imelalamikia vikali kile ilichokitaja kuwa ni kuendelea kwa uvunjifu wa makubaliano ya usitishaji vita na mauaji yanayofanywa na Israel kusini mwa Lebanon, pamoja na kushindwa kwa majeshi ya Israel kuondoa vikosi vyake katika eneo hilo.

Msemaji wa jeshi la Iran amesema kuwa uamuzi huu ni “hatua ya kwanza” katika mfululizo wa maamuzi ya kijeshi yanayolenga kulinda usalama wa kanda hiyo. Iran imetoa onyo kali kwa pande husika, ikisisitiza kuwa hatua zaidi na kali zaidi zitachukuliwa ikiwa ukiukwaji huo utaendelea.

Hali bado ni ya wasiwasi katika eneo hilo muhimu kwa usafirishaji wa mafuta duniani, huku wachambuzi wakionya kuwa hatua hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa dunia na usalama wa kimataifa.

Leave a Reply