JERUSALEM:

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Israel, Ehud Barak, amezua taharuki katika ulingo wa siasa nchini humo kufuatia kauli yake nzito dhidi ya Waziri Mkuu aliyeko madarakani, Benjamin Netanyahu, akimtuhumu kwa njama za kuhujumu demokrasia ili kulinda maslahi yake binafsi.

Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha habari cha Kan News, Barak ameonyesha hofu yake kuwa Netanyahu anaweza kujaribu kuvuruga mchakato wa uchaguzi ujao kwa maslahi yake ya kisiasa. Barak ameenda mbali zaidi na kutoa onyo kali akisema, iwapo jaribio hilo litafanyika, wananchi hawatakuwa na chaguo lingine isipokuwa kumwondoa madarakani kwa nguvu za umma.

“Nina hofu kuwa Netanyahu anaweza kujaribu kuhujumu uchaguzi, na anaweza kufanya hivyo kwa urahisi sana. Akijaribu, hatutakuwa na chaguo lingine isipokuwa kumwondoa kwa mawe na vigongo,” alisema Barak kwa hisia kali.

Vita visivyo na mwisho
Katika uchambuzi wake, Barak amedai kuwa Netanyahu anashikilia msimamo wa kuendeleza vita visivyo na ukomo makusudi. Amesema kuwa kiongozi huyo anafahamu fika kuwa kumalizika kwa mapigano kutafungua njia ya kuharakishwa kwa kesi zinazomkabili mahakamani, jambo ambalo Netanyahu analiepuka kwa gharama yoyote.

Suala la Iran na ‘Kiburi’ cha Netanyahu
Kuhusu makubaliano ya nyuklia ya Iran na mkakati wa Israel dhidi ya nchi hiyo, Barak ameuponda utendaji wa serikali ya sasa kwa maneno mafupi lakini mazito.

“Kwa neno moja: Ni mbaya. Kwa maneno mawili: Ni mbaya sana,” alifafanua Barak. Aliongeza kuwa taifa la Israel hivi sasa linaripa gharama kubwa kutokana na kile alichokiita “kiburi na ukosefu wa maono” wa Netanyahu.

Barak amehitimisha kwa kusema kuwa hakuna hata lengo moja kati ya malengo yaliyowekwa katika vita dhidi ya Iran ambalo limefikiwa, jambo linaloashiria kushindwa kwa diplomasia na mikakati ya kijeshi chini ya uongozi wa Netanyahu.

Kauli hizi za Ehud Barak zinakuja wakati shinikizo la kisiasa likizidi kuongezeka ndani ya Israel, huku kukiwa na migawanyiko kuhusu namna ya kuhitimisha mizozo inayoendelea na hatma ya kisiasa ya Benjamin Netanyahu.

Leave a Reply