TEHRAN, Iran – Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei, ametoa tamko zito akisisitiza kuwa hadhi ya Iran kama taifa lenye nguvu kubwa duniani (superpower) si kauli mbiu tu, bali ni ukweli uliothibitishwa kupitia ushindi wa kijeshi na kidiplomasia.

Akizungumza na waandishi wa habari, Baghaei ameeleza kuwa Iran imefanikiwa kuyashinda mataifa mawili makubwa yenye nguvu za nyuklia, yaliyokuwa yakisaidiwa na kundi la nchi washirika. “Hatupigi kelele za maneno; sisi ni taifa kubwa kwelikweli kwani tumeweza kusimama imara dhidi ya mataifa yenye silaha za nyuklia,” alisema msemaji huyo.

Aidha, Baghaei alitumia sitiari ya kipekee kuwakilisha utambulisho wa nchi hiyo, akisema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ni kama “ngozi” ya Iran. Alibainisha kuwa maadui walikuwa na lengo la “kuichubua” ngozi hiyo ili kuiangamiza nchi, lakini mpango huo umefeli.

Msemaji huyo alihitimisha kwa kusema kuwa jaribio lolote la kutofautisha kati ya “Iran” na “Jamhuri ya Kiislamu” ni dhana potofu na ya kufikirika tu. Alisisitiza kuwa mtu yeyote mwenye mapenzi ya dhati na nchi hiyo anaelewa kuwa nchi na mfumo wake wa utawala ni kitu kimoja kisichotenganika.

Leave a Reply