WASHINGTON D.C. – Mchambuzi wa masuala ya kisiasa nchini Marekani, Tucker Carlson, ametoa kauli nzito inayozua mjadala mpana kuhusu uhusiano wa Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kuhusiana na mzozo wa Iran.
Katika mfululizo wa maelezo yake, Carlson amebainisha kuwa ajenda ya kuingia vitani na Iran imekuwa ikipigiwa debe na Netanyahu kwa zaidi ya miongo mitatu. Carlson anadai kuwa, licha ya marais waliopita wa Marekani kusita, Donald Trump alikuwa kiongozi wa kwanza “kunasa” kwenye kile alichokiita mtego wa muda mrefu.
“Wamekuwa wakizungumzia vita hivi, kama Netanyahu mwenyewe alivyosema, kwa takriban miaka 30 hivi. Na Trump ndiye Rais wa kwanza wa Marekani ambaye kwa hakika alitekeleza hilo. Alitumbukia humo; walimvuta kwenye mtego na yeye akajitosa kichwa kichwa,” alisema Carlson.
Mchambuzi huyo alizidi kufafanua kuwa kwa sasa Trump ametambua jinsi alivyofanywa daraja la kufikia malengo ya wengine na jinsi alivyodanganywa katika mchakato huo. Carlson anaeleza kuwa Trump anaonekana kuwa na kinyongo na uchungu mwingi kutokana na jinsi hali ilivyokuwa.
Aidha, Carlson alihitimisha kwa kusema kuwa Trump sasa anaelewa kwamba, ili kujinasua katika hali hiyo tata, hana budi kufanya makubaliano yoyote yale—hata kama yatakuwa ni makubaliano mabaya—kwa kuwa kwa sasa hana chaguo lingine mbadala la kurejesha utulivu.
Kauli hizi za Carlson zinakuja wakati ambao siasa za Mashariki ya Kati na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Marekani na washirika wake vikiendelea kuwa kitovu cha mivutano ya kimataifa.
