JERUSALEM – Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, ametoa kauli nzito inayozua mjadala mpana, akisisitiza kuwa nchi yake haitafungwa na makubaliano yoyote yaliyofikiwa na Rais wa Marekani, Donald Trump, ikiwa yanakwenda kinyume na maslahi ya nchi hiyo.
Katika taarifa yake aliyoitoa mapema leo, Ben-Gvir ameweka wazi kuwa ingawa Israel inaheshimu na kuthamini uhusiano wake na Marekani, nchi hiyo ni taifa huru lenye mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake yenyewe.
“Makubaliano ya Trump hayatufungi. Israel haiko chini ya mamlaka ya Marekani; sisi ni taifa huru na lenye enzi kamili,” alisema Waziri huyo kwa msisitizo.
Ben-Gvir, ambaye anajulikana kwa misimamo mikali, aliongeza kuwa Israel ina mapenzi ya dhati kwa Taifa la Marekani na inatambua mchango mkubwa wa Rais Trump, lakini akasisitiza kuwa urafiki huo haumaanishi kuwa Israel itapokea maelekezo kama nchi isiyo na nguvu.
“Tunasisitiza hili: Tunaipenda Marekani na tunamshukuru Rais Trump. Hata hivyo, ni lazima ieleweke kuwa Dola ya Israel si ‘Jamhuri ya Ndizi’ (Banana Republic),” alikaririwa Ben-Gvir.
Kauli hii inatafsiriwa na wachambuzi wa mambo kama ujumbe wa wazi kwa washirika wa kimataifa wa Israel kuwa nchi hiyo itatanguliza kwanza kile inachoona ni usalama na mustakabali wake kabla ya kufuata shinikizo lolote la nje.
Hadi sasa, hakujatolewa tamko rasmi kutoka upande wa Donald Trump au serikali ya Marekani kuhusiana na kauli hiyo ya Waziri Ben-Gvir ambayo imeteka vichwa vya habari vya kimataifa.