SEOUL, KOREA KUSINI
Mahakama moja jijini Seoul imemhukumu aliyekuwa Rais wa Korea Kusini kifungo cha miaka 30 gerezani, kufuatia kashfa nzito iliyohusisha uchochezi wa mivutano ya kijeshi dhidi ya jirani yao, Korea Kaskazini.
Katika uamuzi uliotolewa siku ya Ijumaa, mahakama hiyo imemkuta kiongozi huyo wa zamani na hatia ya kutoa amri ya kurushwa kwa ndege za kijeshi zisizo na rubani (drones) katika anga la Korea Kaskazini. Hatua hiyo imetajwa kuwa ililenga makusudi kuongeza uhasama katika Rasi ya Korea, eneo ambalo tayari lina mivutano ya muda mrefu.
Upande wa mashtaka ulithibitisha kuwa lengo kuu la kiongozi huyo lilikuwa ni kutengeneza mazingira ya hofu na mzozo wa kijeshi ili kupata kisingizio cha kutangaza hali ya hatari (Martial Law) nchini humo.
Hukumu hii inatazamwa kama pigo kubwa la kisheria kwa kiongozi huyo, huku mahakama ikisisitiza kuwa vitendo vyake vilihatarisha usalama wa taifa na amani ya kikanda kwa manufaa ya kisiasa.
Hadi sasa, hukumu hiyo imepokelewa kwa hisia tofauti nchini humo, ikihitimisha mfululizo wa kesi zilizokuwa zikifuatiliwa kwa karibu duniani kote kuhusiana na usalama wa Rasi ya Korea.