Hali ya kisiasa nchini Uingereza imekumbwa na mtikisiko mkubwa kufuatia uamuzi wa ghafla wa Waziri wa Ulinzi, John Healey, kujiuzulu nafasi yake mapema Alhamisi ya leo.

Katika barua yake ya kujiuzulu iliyojaa shutuma nzito, Bwana Healey amemnyooshea kidole cha lawama Waziri Mkuu, Keir Starmer, akimtuhumu kwa kushindwa kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya sekta ya ulinzi.

Healey amesisitiza kuwa uamuzi huo wa serikali unaiacha Uingereza katika hali ya hatari na “upungufu mkubwa” wa kijeshi, jambo ambalo amesema ni hatari kwa usalama wa taifa hilo katika kipindi hiki ambacho ulimwengu unakabiliwa na tishio kubwa la amani.

“Hatuwezi kulinda nchi yetu kwa ahadi tupu wakati maadui wanazidi kuimarika. Bajeti ya sasa inaiacha Uingereza nyuma ya mahitaji yake ya msingi ya kujilinda,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo ya Healey.

Kujiuzulu huku kunatajwa kuwa pigo kubwa kwa serikali ya Starmer, ambayo sasa inalazimika kujibu mapigo dhidi ya madai kuwa inahatarisha usalama wa raia kwa kuminya matumizi ya kijeshi.

Hadi sasa, Ikulu ya Uingereza (Downing Street) haijatoa tamko rasmi kufuatia hatua hiyo ya ghafla ambayo imewaacha wadau wa usalama na siasa nchini humo na maswali mengi juu ya mustakabali wa ulinzi wa taifa hilo.

Leave a Reply