WASHINGTON:
Mfuko rasmi unaosimamiwa na Benki ya Dunia chini ya mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kuijenga upya Gaza unaojulikana kama “Bodi ya Amani” (Board of Peace), umeripotiwa kuwa na “dola sifuri” hadi sasa, licha ya kuwepo kwa ahadi za michango zinazofikia takriban dola bilioni 17.

Kwa mujibu wa ripoti iliyochapishwa Mei 27 na gazeti la Financial Times (FT), mpango huo ambao ulitarajiwa kuwa juhudi za kimataifa za kuijenga upya Gaza iliyoharibiwa vibaya, umekwama kutokana na kasoro za kifedha, utata wa kisheria, na ukosefu wa maendeleo yoyote kwenye eneo la tukio.

Msaidizi mwandamizi wa Bunge la Marekani aliiambia FT kuwa, hakuna kiasi chochote cha fedha hizo ambacho kimeingia au kusimamiwa na bodi hiyo. Badala ya kuwekwa kwenye mfuko rasmi ulioungwa mkono na Umoja wa Mataifa, bodi imeamuru michango ielekezwe kwenye akaunti binafsi ya benki ya JPMorgan. Hatua hii imeibua hofu kubwa miongoni mwa wabunge na waangalizi, kwani akaunti hiyo inakosa uwazi na masharti ya utoaji taarifa yaliyowekwa na Benki ya Dunia.

Ripoti zinaeleza kuwa, kiasi kidogo cha fedha kilichotolewa hadi sasa—ikiwemo dola milioni 3 kutoka Morocco na dola milioni 20 kutoka Falme za Kiarabu (UAE)—kimetumika kulipa mishahara ya wafanyakazi, huku mafungu makubwa kwa ajili ya ulinzi na miundombinu yakiwa yamezuiliwa au hayajatumika.
Katika hatua ya kushangaza, Marekani sasa inafikiria mpango wa kuchukua sehemu ya dola bilioni 5 za mapato ya kodi ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina (PA) ambayo kwa sasa yanazuiliwa na Israel, ili kufadhili shughuli za bodi hiyo zinazosuasua. Mpango huu unalenga kuelekeza kodi hizo kwa mamlaka ya mpito inayoongozwa na Marekani huko Gaza, huku kiasi kinachosalia kikitarajiwa kutolewa kwa PA tu endapo itakubali kufanya mabadiliko maalum yanayoshinikizwa na Israel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *