Akiba ya mafuta ghafi na bidhaa za petroli nchini Marekani imeshuka hadi kiwango chake cha chini zaidi katika zaidi ya miongo miwili, huku mzozo unaoendelea na Iran ukiendelea kuathiri masoko ya nishati duniani, gazeti la Financial Times (FT) limeripoti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, jumla ya akiba ya mafuta ghafi na bidhaa zilizochakatwa nchini Marekani ilipungua kwa mapipa milioni 10.6 katika wiki iliyopita, na kufikia mapipa bilioni 1.57, kiwango cha chini zaidi tangu mwaka 2004.
Kupungua huko kumechangiwa na matumizi makubwa ya mafuta ghafi kutoka kwenye akiba, kuongezeka kwa mauzo ya nje kwenda Ulaya na Asia, pamoja na kuendelea kutolewa kwa mafuta kutoka Akiba ya Kimkakati ya Petroli ya Marekani (Strategic Petroleum Reserve).
Wachambuzi wanaonya kuwa bei za mafuta zinaweza kupanda kwa kiasi kikubwa iwapo Mlango wa Bahari wa Hormuz utaendelea kufungwa kwa meli za kubeba mafuta. Aidha, ongezeko la mauzo ya mafuta nje ya nchi linaendelea kuongeza shinikizo kwenye akiba ya ndani ya Marekani.
Kwa sasa, Marekani imekuwa ikichukua nafasi muhimu katika kusaidia kufidia upungufu wa uzalishaji wa mafuta kutoka Mashariki ya Kati. Hata hivyo, wataalamu wa sekta ya nishati wanaonya kuwa uwezo huo wa kufidia upungufu wa soko la kimataifa una mipaka na hauwezi kudumu bila mwisho.