TEL AVIV – Kituo cha televisheni cha Channel 12 cha Israel kimeripoti kuwa jeshi la nchi hiyo limekiri kuwepo kwa hitilafu katika mfumo wake wa kutoa onyo dhidi ya droni za mashambulizi (FPV) zinazotumiwa na makundi ya Muqawama.

Wakati huo huo, gazeti la Haaretz la Israel limeripoti kuwa jeshi hilo limeelezea wasiwasi mkubwa kuhusu tishio la droni hizo zilizosheheni vilipuzi, huku likikiri wazi kuwa halina uwezo madhubuti wa kiutendaji wa kukabiliana nazo.

Chanzo kimoja cha kijeshi kimeliambia gazeti la Haaretz kuwa: “Hili ni tukio ambalo limetushtukiza na kiukweli hatukuwa tumejipanga.” Chanzo hicho kimebainisha kuwepo kwa ongezeko la shinikizo kwa jeshi hilo, linalotoka kwa makamanda, wanajeshi walioko mstari wa mbele, pamoja na familia zao.

Gazeti hilo limefafanua zaidi kuwa, licha ya kuwepo kwa operesheni za ardhini zilizopanuliwa katika maeneo ya kaskazini kwa lengo la kudhibiti urushwaji wa droni kuelekea kwenye makazi ya watu, jeshi lenyewe limekiri kuwa hatua hiyo bado haijafanikiwa kuzizuia ipasavyo.

Badala yake, hatua ya wanajeshi wa Israel kusonga mbele zaidi imezidi kuwaweka hatarini na kuwafanya walengwe kwa urahisi na droni hizo zinazoongozwa kwa mfumo wa mawasiliano wa ‘fiber-optic’, ambazo imeelezwa kuwa ni vigumu sana kuzidungua au kuzizuia kimawasiliano (jamming).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *