Tehran – Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu wa Iran (IRGC) limetangaza kuwa jumla ya meli 23 za kibiashara, zikiwemo meli za mafuta na zile za kubeba makontena, zimepita salama katika Mlango wa Hormuz ndani ya kipindi cha saa 24 zilizopita.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, meli zote zilivuka njia hiyo ya kimkakati baada ya kufanyika uratibu rasmi na mamlaka za wanamaji za IRGC.
Katika taarifa iliyotolewa usiku wa Jumatano, IRGC ilisema inaendelea kusimamia kwa karibu njia hiyo ya baharini, ikieleza kuwa ina udhibiti wa kudumu, thabiti na wenye nguvu katika eneo hilo.
Taarifa hiyo pia iliieleza Ghuba ya Uajemi kuwa ni eneo la bahari linalohusu mataifa ya kanda pekee. Aidha, IRGC ilidai kuwa hali ya sintofahamu ya kiusalama inayoshuhudiwa sasa katika eneo hilo inachangiwa na uwepo pamoja na shughuli za kijeshi za Marekani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, majeshi ya Marekani ndiyo chanzo kikuu cha kuyumbisha utulivu wa eneo hilo.