Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa sehemu muhimu za maelewano yanyolenga kumaliza vita vilivyolazimishwa zinakaribia kukamilika, pamoja na kuwepo misimamo kinzani ya Washington na vitendo vya mara kwa mara vya uchokozi wa kijeshi vinavyolenga kuvuruga mchakato wa kidiplomasia.

Katika mahojiano jioni ya Alhamisi, Esmaeil Baghaei amekanusha uvumi wa vyombo vya habari kuhusu kufikiwa kwa makubaliano na akasisitiza tena msimamo thabiti na wa kimsingi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baghaei amesema, “Kwa upande wa maandishi, rasimu ya makubaliano imekaribia kukamilika katika sehemu zake kuu. Tatizo ni kwamba misimamo kinzani ya Marekani imekuwa mara kwa mara chanzo cha misukosuko na kuvuruga mchakato huu.”

Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu iliingia katika mchakato wa kidiplomasia kwa nia njema na kwa uwajibikaji kamili, huku maafisa wa Marekani wakibadili mara kwa mara misimamo yao, wakitoa madai mapya yasiyo ya uhalisia, na hata kufanya mashambulizi ya kijeshi wakati mazungumzo yakiendelea.

Baghaei amebainisha kuwa tangu tangazo la usitishaji mapigano mwezi Aprili, Marekani na utawala wa Israel wamekiuka mara kadhaa makubaliano hayo ya kusitisha vita.

Katika mashambulizi ya hivi karibuni, vikosi vya Marekani vililenga miundombinu ya kusini mwa Iran na kushambulia mabwawa mawili ya maji katika eneo la Sirik, kitendo ambacho ni jinai ya kivita.

Amesisitiza wazi kwamba Iran imeonyesha, katika diplomasia na pia katika uwanja wa mapambano, kwamba haitakubali kamwe masharti na matakwa ya upande wa pili.

Baghaei amesisitiza kuwa: “Iran imeonyesha kwa vitendo kwamba mistari yake myekundu ni maslahi na ustawi wa taifa la Iran, na hakutakuwa na maafikiano yoyote yanayokiuka hilo.”

Ameongeza kuwa: “Lau Jamhuri ya Kiislamu ingekuwa na nia ya kurudi nyuma kutoka katika misimamo yake ya kimsingi chini ya shinikizo na vitisho, ingefanya hivyo mwaka mmoja na nusu uliopita. Tumeonyesha kwamba tunasimama imara.”

Leave a Reply