PRETORIA, AFRIKA KUSINI: Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa, ametoa onyo kali dhidi ya makundi ya raia wanaojichukulia sheria mkononi kwa kuwasimamisha na kuwakagua vitambulisho raia wa kigeni mitaani.
Akihutubia taifa kufuatia kuongezeka kwa taharuki na vitisho dhidi ya wahamiaji, Rais Ramaphosa amepiga marufuku vitendo hivyo na kusisitiza kuwa serikali haitavumilia uvunjifu wa amani. Amesema kuwa hakuna raia au kikundi cha kijamii chenye mamlaka ya kisheria ya kuhoji uhalali wa mgeni mtaani, kwani jukumu hilo ni la vyombo vya dola.
Hotuba hii imekuja kufuatia tishio la baadhi ya makundi yaliyoweka msimamo wa kuwataka wahamiaji wasio na nyaraka kuondoka nchini humo ifikapo Juni 30, 2026. Rais ameonya kuwa changamoto za ndani, ikiwemo ukosefu wa ajira, zisitumike kama kisingizio cha kuchochea chuki na vurugu.
“Ninajua kuwa Waafrika Kusini si watu wanaochukia wageni. Hatupaswi kushawishiwa na wale wanaotaka tuwageuke watu ambao hawakuzaliwa katika nchi hii,” alisisitiza kiongozi huyo.
Rais amehitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kudumisha amani na kufuata taratibu za kisheria badala ya kujiingiza kwenye vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa nchi na taswira ya Afrika Kusini kimataifa.