RONGAI KENYA, The clinical officer at Ray Drop-In Centre demonstrates the range of anti-retrovirals they can provide to clinic clients. (c) Nell Freeman for the Alliance

NAIROBI, KENYA – Wimbi la ghadhabu na malalamiko makubwa limeikumba nchi kufuatia ripoti ya kushtusha kuwa shehena ya dawa na vifaa muhimu vya matibabu vyenye thamani ya shilingi milioni 377 vimeharibika katika maghala ya Mamlaka ya Kusambaza Dawa Nchini (KEMSA).

Inaarifiwa kuwa dawa hizo zimevuka muda wake wa matumizi (expiry) zikiwa bado zimehifadhiwa ghalani, jambo ambalo limezua maswali mazito kuhusu usimamizi wa rasilimali za umma katika sekta ya afya.

Dawa zilizoharibika ni pamoja na zile za kutibu ugonjwa wa saratani, dawa za kufubaza makali ya virusi vya UKIMWI (ARVs), pamoja na bidhaa nyingine muhimu ambazo ni tegemeo kwa maisha ya maelfu ya Wakenya.
Kilio cha Mwananchi wa Kawaida

Hali hii inatokea wakati ambapo sekta ya afya nchini inakabiliwa na changamoto tele. Katika kipindi ambacho dawa hizi zilikuwa zikioza ghalani, maelfu ya wagonjwa katika hospitali za umma kote nchini walikuwa wakirejeshwa nyumbani bila matibabu kwa kile kinachoelezwa kuwa “ukosefu wa dawa.”

Wagonjwa wengi wasio na uwezo walilazimika kupenya mifukoni mwao kununua dawa hizo kwa bei ghali katika maduka ya dawa ya kibinafsi, huku wale wasio na fedha wakibaki kuteseka majumbani mwao.

Uzembe au Changamoto za Mfumo?

Wadau wa sekta ya afya na wanaharakati wameitaka serikali kutoa maelezo ya kina jinsi dawa za thamani hiyo kubwa zinavyoweza kuachwa ziharibike ilhali hitaji ni kubwa mahospitalini. Kashfa hii imeweka KEMSA kwenye darubini tena, huku kukiwa na shinikizo kwa maafisa waliohusika kuwajibishwa kwa kile kinachotajwa kuwa ni uzembe uliokithiri na ubadhirifu wa kodi za wananchi.

Hadi sasa, usimamizi wa KEMSA unakabiliwa na shinikizo la kueleza ni kwa nini mfumo wa usambazaji ulishindwa kufikisha dawa hizo kwa walengwa kwa wakati unaofaa, huku maisha ya Wakenya wanyonge yakiendelea kuwekwa rehani.

Leave a Reply