TEHRAN, IRAN – Serikali ya Iran imeweka wazi kuwa hakuna dalili zozote za kufikia makubaliano ya haraka na Marekani, ikisisitiza kuwa tofauti kati ya mataifa hayo mawili ni kubwa, nyingi, na zenye mizizi mirefu ambayo haisuluhishiki kwa urahisi.
Akitoa ufafanuzi huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bw. Ismael Baqaei, amesema kuwa ni vigumu kutarajia suluhu ya haraka kupitia vikao vichache. “Hatuwezi kusema tumefikia hatua ambayo makubaliano yapo karibu. Hapana, hali haiko hivyo. Tofauti kati ya Iran na Marekani ni kubwa sana na hazisuluhishiki kwa urahisi.
Hatuwezi kusema kwa uhakika kwamba baada ya ziara chache au mazungumzo ya wiki au miezi kadhaa, tutafikia muafaka,” alisema Bw. Baqaei.
Akigusia suala la mpango wa nyuklia wa taifa hilo, Msemaji huyo alisisitiza kuwa Iran ni mwanachama halali wa Mkataba wa Kuzuia Usambazaji wa Silaha za Nyuklia (NPT) na hivyo ina haki ya msingi ya kurutubisha uraniamu. Aliongeza kuwa msimamo wa taifa hilo kuhusu akiba yake ya uraniamu iliyorutubishwa uko wazi na unajulikana.
Hata hivyo, Bw. Baqaei alifafanua kuwa mazungumzo yanayoendelea kwa sasa hayaingii kwa undani kwenye masuala ya kiufundi ya nyuklia, kwani kufanya hivyo kunaweza kukwamisha juhudi za kupata suluhu.”Maelezo ya kina kuhusiana na suala la nyuklia hayajadiliwi katika hatua hii, na kwa hakika hatutafikia suluhu yoyote ikiwa tutajaribu kuchimba kwa kina kuhusu akiba yetu ya uraniamu iliyorutubishwa,” alihitimisha.