Serikali ya Qatar imetoa tamko kali la kulaani kitendo cha Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel cha kuwatesa na kuwanyanyasa wanaharakati wa kundi la Global Sumud Flotilla waliotiwa mbaroni na mamlaka za Israel.

Katika taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, hatua hiyo imetajwa kuwa ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na kitendo kisicho na chembe ya ubinadamu.

Wizara hiyo imesema kuwa unyanyasaji huu, unaofanywa hadharani dhidi ya wanaharakati kutoka mataifa yenye uhusiano na Israel, ni kielelezo tosha cha mateso ya kila siku wanayopitia wananchi wa Palestina chini ya mfumo wa ukaliaji na ubaguzi wa rangi kwa miongo mingi sasa.

Qatar imesisitiza kuwa vitendo vya mawaziri katika serikali ya Israel havipaswi kutazamwa kama matukio ya kujitegemea, bali ni sehemu ya sera rasmi ya kimfumo ambayo haina heshima kwa utu wa binadamu wala haijali sheria za kimataifa au wito wa jumuiya ya kimataifa.

Kufuatia hali hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imeitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua za haraka na za dharura ili kusitisha uchokozi wa Israel, kuwataka wanaharakati hao waachiliwe huru mara moja na bila masharti yoyote.

Mwisho, Qatar imesisitiza kuwa ni wakati muafaka kwa mamlaka ya ukaliaji kuwajibishwa kwa uhalifu wake wa muda mrefu dhidi ya Wapalestina, na kukomesha utamaduni wa kutokujali sheria ambao umekuwa ukichochea vitendo hivyo kuendelea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *