Saudi Arabia imeanza kujiondoa katika baadhi ya miradi yake mikubwa ya uwekezaji, hasa katika sekta ya michezo, kwa mujibu wa ripoti ya gazeti la The New York Times.
WKatika kipindi cha takribani muongo mmoja uliopita, nchi hiyo chini ya uongozi wa Mwanamfalme Mohammed bin Salman iliwekeza fedha nyingi katika michezo na burudani ikiwa ni sehemu ya juhudi za kupunguza utegemezi wa uchumi wake kwa mafuta na kuboresha taswira yake kimataifa.
Hata hivyo, kupungua kwa mapato ya mafuta, kuongezeka kwa gharama za matumizi, pamoja na shinikizo la mizozo ya kikanda, kumesababisha baadhi ya miradi hiyo kupunguzwa au kusimamishwa.
Miongoni mwa miradi inayotajwa ni mradi wa mashindano ya gofu wa LIV, ambao ulianzishwa kwa uwekezaji wa mabilioni ya dola na ulihusisha ushiriki wa wachezaji mashuhuri. Saudi Arabia imeripotiwa kutangaza kuwa haitauendelea kuufadhili mradi huo baada ya mwisho wa mwaka huu.
Hatua hiyo inaashiria mabadiliko ya mkakati wa kiuchumi wa Saudi Arabia, ambapo sasa inaelekeza zaidi nguvu katika uwekezaji wa ndani na kuongeza ufanisi wa matumizi—jambo linaloweza pia kuwa na athari katika sekta ya michezo duniani.