TEHRAN, IRAN

Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, amekanusha vikali madai yaliyotolewa na serikali ya Marekani (Washington) kwamba Iran inapanga kutumia fedha zake zilizokuwa zimezuiliwa kwa ajili ya kununua bidhaa za kilimo kutoka nchini Marekani.

Akijibu madai hayo kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), Ghalibaf alitumia lugha ya dhihaka na picha kuelezea uhusiano wa sasa kati ya mataifa hayo mawili.

Ghalibaf aliandika: “Inashangaza. Zao pekee tunalovuna sasa hivi ni lile mlilopanda ninyi wenyewe: miongo kadhaa ya kutoaminiana.”

Kiongozi huyo aliendelea kufafanua kuwa “zao” hilo la kutoaminiana ni la asili, limejaa tele, na limeoteshwa nchini mwao kutokana na vitendo vya Marekani. Katika kile kinachoonekana kama shambulio la maneno dhidi ya ubora wa bidhaa na diplomasia ya Marekani, Ghalibaf aliongeza kuwa Marekani haina kingine cha kusafirisha nje isipokuwa soya za GMO (zilizobadilishwa vinasaba), ahadi zilizovunjika, na maneno ya kejeli.

Kauli hii ya Ghalibaf imekuja wakati kukiwa na mivutano ya kidiplomasia kuhusu namna Iran itakavyotumia mabilioni ya dola ya mali zake ambazo zilikuwa zimezuiliwa nje ya nchi kutokana na vikwazo, na sasa zimeanza kuachiwa.

Wakati Washington ikidai kuwa fedha hizo zinaweza kutumika kwa mahitaji ya kibinadamu ikiwemo chakula na kilimo, Tehran imesisitiza kuwa ina mamlaka kamili ya kuamua jinsi ya kutumia rasilimali zake bila kuingiliwa na nchi za Magharibi.

Leave a Reply