Joto la kisiasa linaanza kupanda katika Kaunti ya Mombasa huku maandalizi ya uchaguzi mkuu wa 2027 yakianza kuchukua mwelekeo mpya, hasa katika kinyang’anyiro cha ugavana. Mchuano huo unatarajiwa kuwa mkali, ukihusisha viongozi wenye ushawishi mkubwa katika eneo la Pwani.
Miongoni mwa wanaotajwa sana katika mbio hizo ni Mbunge wa Nyali Mohamed Ali, maarufu kama Jicho Pevu.
Mwanasiasa huyo, ambaye amekuwa sauti ya kipekee katika siasa za Mombasa, anajiandaa kufanya jaribio jipya la kuwania uongozi wa kaunti hiyo katika uchaguzi ujao wa 2027.
Katika azma hiyo, Bw Ali anatarajiwa kuwania ugavana kupitia chama cha Wiper Democratic Movement.
Hata hivyo, safari yake haitakuwa rahisi kwani atakutana na ushindani mkali kutoka kwa Waziri wa Madini na Uchumi wa Bahari Hassan Joho pamoja na gavana wa sasa Abdulswamad Nassir.
Aidha, viongozi wengine kadhaa waliochaguliwa katika kaunti hiyo pia wanatajwa kuwania wadhifa huo, hali inayofanya kinyang’anyiro hicho kuwa miongoni mwa vyenye ushindani mkubwa zaidi katika eneo la Pwani.
Ushindani huo pia unaangaliwa kama mtihani muhimu kwa chama cha Orange Democratic Movement (ODM), ambacho kwa muda mrefu kimekuwa kikitawala siasa za Mombasa. Viongozi wa chama hicho wanataka kuthibitisha kuwa kaunti hiyo bado ni ngome yao licha ya mabadiliko ya kisiasa yanayoendelea nchini na kuongezeka kwa ushirikiano kati ya baadhi ya viongozi wa upinzani na Rais William Ruto.
Akizungumza hivi karibuni, Bw Joho alisisitiza kuwa ODM itaendelea kuwa na ushawishi mkubwa katika eneo la Pwani. “Tunaamini Mombasa na eneo lote la Pwani bado ni ngome za ODM.
Kuhusu urais tuko pamoja na Rais William Ruto, lakini katika nafasi nyingine tutahakikisha ODM inasalia madarakani kote katika eneo hili,” alisema Bw Joho.Kwa upande wake, Bw Ali anaona uchaguzi wa 2027 kama fursa ya kurejea mkakati uliomwezesha kuvunja nguvu ya mashine ya ODM katika chaguzi zilizopita. Mbunge huyo amejijengea sifa kupitia mapambano dhidi ya ufisadi, msimamo wa uwazi katika uongozi na mtazamo wa kisiasa usioegemea upande wa viongozi wakuu.
Amesalia kuwa miongoni mwa viongozi wachache waliochaguliwa Mombasa wanaofuata mkondo wao wa kisiasa, wakati gavana, seneta na wabunge wengi wa kaunti hiyo wamejiunga na viongozi wanaounga mkono serikali ya Rais Ruto.
Bw Ali pia amekuwa mkosoaji wa kile anachokiita vita vya kuchagua dhidi ya ufisadi, akiwatuhumu baadhi ya viongozi kwa kuweka mbele maslahi yao ya kisiasa badala ya kuwahudumia wananchi.“Simba hawaendi pamoja na kondoo.
Ninafuata njia yangu mwenyewe ambayo naamini inalenga maslahi ya wananchi na si kuwa mtumwa wa mwanasiasa fulani,” alisema Bw Ali.