NEW YORK, MAREKANI
Upepo wa kisiasa ndani ya Chama cha Democratic nchini Marekani unaonekana kuchukua mkondo mpya baada ya wanasiasa watatu, ambao wamejenga utambulisho wao kupitia ukosoaji mkali dhidi ya Israel, kuibuka na ushindi wa kishindo katika kura za maoni za chama hicho (primaries) jijini New York siku ya Jumanne.
Ushindi wa wagombea hao unatajwa kuwa ishara tosha ya kuanza kwa enzi mpya ya mashaka na mitazamo tofauti ndani ya chama hicho dhidi ya nchi ya Israel na hatua zake za kijeshi na kisiasa. Kwa muda mrefu, uungaji mkono kwa Israel umekuwa ni mhimili mkuu wa sera za kigeni za Marekani, lakini matokeo haya yanaashiria mabadiliko ya kifikra miongoni mwa wapiga kura wa chama hicho.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa nchini humo wanaeleza kuwa ushindi huo uliopatikana katika maeneo muhimu ya New York City, unaonyesha jinsi ambavyo hoja za kutaka mabadiliko ya sera kuelekea Mashariki ya Kati zinavyozidi kupata nguvu na mashiko kwa umma.
Matokeo haya yanatarajiwa kuleta mjadala mpana ndani ya bunge la Marekani (House of Representatives), huku kizazi kipya cha wanasiasa kikionekana kutoogopa kuhoji ushirika wa kihistoria kati ya Washington na Tel Aviv.