WASHINGTON, MAREKANI
Aliyekuwa Rais wa Marekani, Barack Obama, ametoa kauli nzito akikosoa vikali sera za Donald Trump, kuhusiana na mzozo kati ya Marekani na Iran. Katika kile kinachoonekana kama tathmini ya kina, Obama amesema kuwa mbinu za mabavu na mashambulizi ya kijeshi zimeshindwa kuleta matokeo yoyote ya maana.
Obama amesisitiza kuwa Marekani “haikupata chochote” kupitia sera za vitisho na mashambulizi ya mabomu, na badala yake, hatua bora inayoweza kufikiwa kwa sasa ni kurejea katika makubaliano ya awali ya nyuklia. Ameweka wazi kuwa makubaliano yoyote yatakayofikiwa huko mbeleni hayawezi kuwa bora kuliko lile la JCPOA, ambalo Marekani ilijiondoa kwa kile alichokiita “uamuzi wa kijinga,” licha ya makubaliano hayo kufanya kazi kwa ufanisi kwa miaka mingi.
“Ninatumaini mashambulizi haya yasiyo na tija yatakoma haraka iwezekanavyo,” alisema Obama, huku akiongeza kuwa ni raia wa kawaida ndio wanaozidi kulipa gharama ya mateso kutokana na vita hivyo alivyoviita “vita vya hiari.”
Aidha, kiongozi huyo wa zamani ametoa onyo kwa wale wanaoamini kuwa suluhu inaweza kupatikana kwa kuitishia au kuipiga bomu nchi nyingine. Obama ameyataja mawazo hayo kuwa ni “ndoto ya mchana na udanganyifu” unaotumiwa na watu wenye msimamo mkali, lakini kiuhalisia hayana nafasi katika utatuzi wa migogoro ya kimataifa.
Akihitimisha hoja yake, Obama ametoa wito wa kupewa kipaumbele kwa diplomasia. Amesema kuwa ukweli uliopo unathibitisha kuwa makubaliano ya kisiasa—hata kama yatatatua asilimia 80 hadi 90 tu ya matatizo—ni bora mara maelfu kuliko kuitumbukiza dunia katika vita vya maangamizi visivyo na mwelekeo wala tija.