Katika kauli yenye ukali dhidi ya sera za Rais wa Marekani Donald Trump, Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani amesema kwamba vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran havina uhalali wa maadili.
Papa Leo wa Kumi na Nne amesema kuwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran havitimizi viwango vya “vita vya haki” kwa mujibu wa mafundisho ya Katoliki, akirudia msimamo aliowahi kutoa hapo awali wakati wa ziara yake mjini Madrid.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari wikiendi akiwa safaraini kutoka Roma kuelekea Madrid, Kiongozi wa Kanisa Katoliki amesema: “Katika suala la Iran, vigezo vya kuhalalisha vita vya haki havipo.”
Ameongeza kuwa nadharia ya jadi ya vita vya haki iliundwa katika kipindi ambacho binadamu hangeweza kufikiria kiwango cha uharibifu wa silaha za kisasa.
Kauli hizi zinakuja baada ya tofauti za awali na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance, ambaye alikuwa ametetea mzozo huo kama “vita vya haki”, jambo ambalo Papa alilikataa.
Wakati Marekani na Israeli zilipoanzisha vita haramu dhidi ya Iran Februari 28,, Papa Leo alitoa wito mara kwa mara wa kusitishwa kwa vita na kukosoa kauli kali ambazo alisema zinaweza kuchochea kuongezeka zaidi kwa mvutano.
Katikati ya vita hivyo vilivyoendelea kwa siku 40, alielezea tishio la Donald Trump kwamba “ataangamizwa ustaarabu wa Iran” kuwa kauli isiyokubalika.
Trump baadaye alijibu kwa kumtaja papa kuwa “dhaifu na mbaya sana katika masuala ya sera ya kigeni.”
Papa alikataa ukosoaji huo, akisema hana hofu na ataendelea kuzungumza dhidi ya vita. Katika moja ya hotuba zake, alikosoa vikali vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, akivitaja kuwa ni fedheha kwa familia nzima ya kibinadamu na mtihani mkubwa wa maadili kwa ulimwengu mzima.
Mabadilishano hayo ya kauli pia yalizua mijadala nchini Italia, ambapo baadhi ya viongozi wa kisiasa walikosoa vikali matamshi ya Trump na kuonyesha uungaji mkono kwa wito wa papa wa kutafuta amani.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alielezea kauli zilizoelekezwa kwa Papa Leo kuwa “hazikubaliki.”