VATIKAN – Papa Leo XIV ametoa tamko zito kuhusu mivutano ya kijeshi katika ukanda wa Mashariki ya Kati, akisisitiza kuwa mashambulizi ya kijeshi yanayofanywa na Marekani na Israel dhidi ya Iran hayawezi kuhalalishwa kama ‘vita vya haki’ (just war).
Katika ujumbe wake, Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani amesema kuwa nadharia ya kale ya vita vya haki – kanuni iliyotumika kwa karne nyingi kuhalalisha mapigano – haikidhi tena uhalisia wa vita vya kisasa ambavyo mara nyingi huleta madhara makubwa kwa wasiohusika na kusababisha maafa yasiyoweza kudhibitiwa.
Papa Leo amesisitiza kuwa katika mazingira ya sasa, matumizi ya nguvu za kijeshi yanapaswa kuepukwa, akionya kuwa hatua za kijeshi zisizo na misingi thabiti ya kimaadili zinazochukuliwa na mataifa makubwa dhidi ya Iran, ni ukiukaji wa kanuni za utu na amani ya kimataifa.
Tamko hili la Papa Leo XIV linatazamwa kama msukumo mpya wa kidiplomasia na kiroho kwa mataifa yanayohusika, huku likihoji uhalali wa hatua za kijeshi zinazochochea sintofahamu zaidi katika eneo hilo ambalo tayari linakabiliwa na migogoro mingi.