Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Heche, amesema amepokea taarifa kutoka kwa mdogo wa Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, kuwa Lissu anaumwa tumbo na anapata maumivu makali tangu jana.
Heche alitoa kauli hiyo Mei 17, 2026 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Nyankumbu, Kata ya Nyankumbu, Wilaya na Mkoa wa Geita.
Amesema mdogo wa Lissu aitwaye Vicent alimpa taarifa kwa njia ya simu kuwa Lissu alianza kuumwa tumbo tangu jana jioni na anaendelea kupata maumivu makali, hali inayozua wasiwasi kwa viongozi na wanachama wa chama hicho.
Heche ameongeza kuwa chama hicho kimesisitiza mara kadhaa kuwa endapo kiongozi wao atapata madhara akiwa gerezani, hali hiyo haitavumilika.
“Tukiwa njiani kuja hapa nimepigiwa simu na mdogo wake Lissu aitwaye Vicent akiniambia kuwa tangu jana jioni Mwenyekiti wetu anaumwa sana tumbo. Tumbo linamkata na ana maumivu makali sana. Tumesema tena na tena, Lissu akipata shida haitaeleweka nchi hii,” amesema Heche.