Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe Dkt. Benson Bagonza amesema Kanisa hilo halijawahi kukaa kikao chochote cha kupanga Rais ajae wala hakuna Dhehebu lenye uwezo wa kuchagua nani awe Rais.
Askofu Dkt. Bagonza ametoa kauli hiyo wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Dayosisi maarufu ‘KAD DAY’ ambapo Mgeni rasmi alikuwa ni Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Uhusiano, Deus Sangu.
“Kitengo chako cha mahusiano kinayahusisha Makanisa, Misikiti na makundi yote ya kiimani, sisi sote wa Makanisa tupo chini yako kwa ajili ya uratibishaji wa mahusiano na makundi haya ya imani ni muhimu kwa sababu ndani yake kuna Vyama vyote, Makabila yote, Rangi zote, Maskini na Matajiri.”
“Sisi kama KKKT hatujawahi kukaa kikao chochote kupanga Rais ajaye, hatujawahi na hatuna mpango huo kwani tunaamini hakuna Dhehebu lolote Nchini lenye uwezo wa kutuchagulia Rais, nayasema haya ili kukemea njama ya kuchafua Kanisa letu kwamba tunapanga kuweka Rais mwaka 2030” Askofu Dkt.Bagonza.