Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye ambaye ni Mwenyekiti wa Kiduru wa Umoja wa Afrika amewaalika wapinzani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo katika mazungumzo yanayolenga kujadili mgogoro wa DRC.
Muungano wa Kifungu cha 64, unaowaleta pamoja viongozi kadhaa wa upinzani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, umeahirisha maandamano yake ya amani, ambayo awali yalipangwa kufanyika Julai 8, hadi Julai 22.
Katika taarifa iliyotolewa siku ya Ijumaa, C64 ilitangaza kwamba imekubali mwaliko kutoka kwa Rais wa Burundi Évariste Ndayishimiye, mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Afrika, kwa ajili ya mashauriano kuhusu mgogoro wa kisiasa, usalama, na taasisi nchini DRC. Maelezo ya mpango huu bado hayajaeleweka.
Mbali na C64, mwaliko huo pia umetolewa kwa mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel Denis Mukwege, pamoja na Baraza Kuu la Maaskofu wa kanisa Katoliki na Kanisa la Kristo nchini Kongo. Kambi ya Joseph Kabila, ambayo inapinga jukumu la Burundi katika mgogoro wa usalama mashariki, pia ilitangazwa kushiriki kikao hiki, lakini ilisema siku ya Ijumaa jioni kwamba haijapewa mwaliko wowote.
Jean-Marc Kabund alikuwa wa kwanza kuondoka Kinshasa siku ya Ijumaa jioni, siku mbili baada ya kupokea mwaliko huo. Viongozi wengine wa Muungano wa Kifungu cha 64 wanatarajiwa leo Jumamosi huko Gitega, Burundi.
Miongoni mwao ni Delly Sesanga, ambaye aliweza kupata pasipoti yake, ambayo ilikuwa imechukuliwa siku chache zilizopita na Kurugenzi Kuu ya Uhamiaji.