NEW DELHI, INDIA — Ripoti mpya ya kituo cha habari cha Al Jazeera imefichua kuwa wanawake wa Kiislamu nchini India wanawalenga kwa udhalilishaji mkubwa wa kijinsia na propaganda za uongo kupitia teknolojia ya Akili Mnemba (Generative AI) kwenye mitandao ya kijamii. Mtindo huu, unaochochewa na chuki za kidini, unatumia picha na video bandia za ngono kuwachafua waathiriwa, huku sheria za sasa za nchi hiyo zikiwa hazina uwezo wa kuzuia kasi na ukubwa wa mashambulizi hayo.

Utafiti uliofanywa na Kituo cha Uchunguzi wa Chuki Iliyoratibiwa (CSOH) cha mjini Washington, D.C., ulikagua picha na video 1,326 za AI kutoka kurasa 297 za mitandao ya X, Facebook, na Instagram kati ya Mei 2023 na Mei 2025. Matokeo yalionyesha kuwa maudhui hayo machafu yaliyolenga wanawake wa Kiislamu yalizalisha mwingiliano (interactions) zaidi ya milioni 6.7, huku yakionyesha taswira ya wanawake hao wakiwa na wanaume wa Kihindu, na kuwapaka matope wanaume wa Kiislamu kama watu wenye vurugu.

“Akili Mnemba imefanya uwezekano wa kubadilisha fikra za ngono kuwa picha halisi kwa kasi kubwa na bila gharama yoyote,” alisema Zenith Khan, mwandishi mwenza wa utafiti huo wa CSOH.

Miongoni mwa waathiriwa wa janga hili ni Samreen Ayoub (24), mwanamitindo kutoka jimbo la Kashmir linalodhibitiwa na India. Ayoub aligundua video yake ya uongo iliyosambazwa Instagram ikidai anajiuza kwa wanaume wa Kihindu, ikitumia picha zake za zamani na sauti iliyotengenezwa na AI.

“Ilihisi kama kushambuliwa hadharani kidijitali (digital lynching),” Ayoub aliiambia Al Jazeera. Alieleza kuwa alipoteza fursa zote za kazi kwa takriban miezi mitano na juhudi zake za kuripoti polisi hazikusaidia.

Pengo la Kisheria na Athari zake
Changamoto kubwa inasalia katika sheria ya Teknolojia ya Habari ya India (IT Act Section 66E). Ingawa sheria hiyo inazuia usambazaji wa picha za utupu bila ridhaa, haifanyi kazi ipasavyo pale ambapo picha au video hizo zimetengenezwa na AI na hakuna mwili halisi wa mtu uliorekodiwa. Aidha, mitandao ya kijamii inalindwa kisheria dhidi ya kubeba lawama iwapo tu itaondoa maudhui hayo baada ya kupewa taarifa, hatua ambayo waathiriwa wengi wanashindwa kuifikia.

Kufuatia hali hii, kituo cha usaidizi cha Mumbai, ‘Meri Trustline’, kimesema kimeshughulikia zaidi ya kesi 482 za udhalilishaji, ambapo asilimia 10 inahusisha maudhui yaliyodanganywa kidijitali—idadi ambayo inaongezeka kwa kasi. Wadau wa haki za binadamu sasa wanatoa wito wa kufanyiwa marekebisho ya haraka kwa sheria za nchi hiyo ili kudhibiti matumizi mabaya ya AI kabla hayajaleta madhara makubwa zaidi ya kijamii.

Leave a Reply