Rais wa Urusi, Vladimir Putin, ameamua kuhamisha jeti yake ya kifahari ya Graceful yenye thamani ya dola milioni 133 kutoka maji ya Ulaya kuelekea bandari ya Murmansk iliyoko Kaskazini mwa Urusi. Hatua hiyo inakuja kufuatia wasiwasi mkubwa wa usalama, huku kukiwa na tishio la mashambulizi ya droni kutoka kwa jeshi la Ukraine.
Chombo hicho chenye urefu wa mita 82, kinasindikizwa na meli ya kivita yenye silaha nzito ya aina ya Severomorsk, pamoja na meli nyingine ya doria ya Voevoda. Safari hii inakuja wakati ambapo uchambuzi wa kiusalama unaonyesha kuwa vituo vya majini vya Urusi viko hatarini, hasa baada ya mashambulizi ya hivi karibuni ya droni za Ukraine yaliyoharibu meli ya kisasa ya RFS Boiky katika kituo cha Kronstadt.
Wachambuzi wa masuala ya usalama wa Magharibi wanaelezea hatua hii ya Urusi kama “ulinzi uliopitiliza,” wakisema Kremlin inachukua kila tahadhari kuzuia chombo hicho kisiharibiwe au kuzuiwa na nchi za Magharibi.
Ripoti zinaonyesha kuwa Graceful ilizima mfumo wake wa utambulisho (AIS) mara tu ilipoingia katika Bahari ya Kaskazini ili kuficha mienendo yake, huku ikipita karibu na pwani ya Norway chini ya uangalizi wa karibu wa NATO.
Hatua hii ni sehemu ya mfululizo wa hatua za kiusalama zinazoimarishwa na Kremlin. Taarifa kutoka ndani ya Urusi zinasema kuwa mfumo wa ulinzi wa rais umepanuliwa na sasa una walinzi zaidi ya 800, huku makazi ya rais ya Ziwa Valdai yakizingirwa na mifumo ya kisasa ya makombora ya Pantsir kuzuia mashambulizi ya angani.
Hii si mara ya kwanza kwa mali ya uongozi wa Urusi kuhamishwa. Hivi karibuni, meli nyingine ya kifahari ya Victoria iliondoka katika Bahari Nyeusi kuelekea Bodrum, Uturuki, kutafuta hifadhi kutokana na vikwazo vya kimataifa na vitisho vya kivita.
Chanzo: The Telegraph