TEHRAN, IRAN– Mkuu wa Idara ya Huduma za Dharura katika Mkoa wa Tehran, Mohammad Ismail Tavakoli, amewahakikishia wananchi kuwa hali ya usalama wa raia imeimarika na hakuna majeruhi yeyote aliyeripotiwa kufuatia matukio ya hivi karibuni.

Akizungumza mapema leo kutoa tathmini ya hali ya dharura mkoani humo, Tavakoli amesema kuwa licha ya tahadhari zilizochukuliwa kufuatia mfululizo wa mashambulizi ya hivi karibuni, rekodi za hospitali na vituo vya dharura zinaonyesha kuwa hakuna mtu aliyepata madhara ya kimwili.

“Alhamdulillah, mpaka wakati huu tunapozungumza, hatujapokea ripoti ya majeruhi yeyote katika mkoa mzima wa Tehran kufuatia matukio haya ya hivi karibuni,” alisema kiongoziه huyo.

Hata hivyo, Tavakoli amebainisha kuwa maafisa wa usalama na uokoaji hivi sasa wanachunguza matukio mawili ya milipuko yaliyoripotiwa. Amesema uchunguzi wa kina unafanyika na taarifa rasmi zitatolewa kwa vyombo vya habari punde tu undani wa milipuko hiyo utakapobainika.

Kuhusu utendaji wa idara yake, mkuu huyo ameeleza kuwa idadi ya simu za dharura zinazopokewa haijaongezeka ikilinganishwa na siku za kawaida, jambo linaloashiria utulivu miongoni mwa wakazi.

Aidha, amesisitiza kuwa kikosi kizima cha magari ya dharura (ambulanzi), kikishirikiana na sekta binafsi, kipo katika hali ya tahadhari ya juu na kimejipanga kikamilifu kutoa huduma kwa wananchi wakati wowote hitaji likitokea.

Leave a Reply