Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira, amesema Tanzania iko tayari kupokea ushauri kutoka kwa washirika wa kimataifa, lakini haitakubali maagizo yanayoingilia masuala yake ya ndani.w
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira, amepinga kauli na msimamo wa Jumuiya ya Madola kuhusu masuala ya ndani ya Tanzania, akisema nchi hiyo ni huru na haiwezi kuamrishwa namna ya kuendesha taasisi zake.
Akizungumza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha ITV siku ya Jumanne, Wasira alisema Tanzania haijajitenga na jumuiya ya kimataifa na iko tayari kusikiliza ushauri kutoka kwa washirika mbalimbali, lakini alisisitiza kuwa maamuzi ya ndani yanapaswa kubaki chini ya mamlaka ya nchi.
“Hatujakataa kuridhiana, lakini Jumuiya ya Madola haiwezi kutuamrisha kuingilia Mahakama. Kuna mambo wanaweza kutushauri na hatukatai kushauriwa, lakini haiwezi kutuamrisha, inakuwa inatuingilia uhuru wetu,” alisema Wasira.
Aliongeza kuwa Tanzania ina uhusiano na mataifa na jumuiya mbalimbali duniani, akitaja Umoja wa Ulaya, Marekani, Urusi na China kama baadhi ya washirika ambao nchi hiyo inaweza kushirikiana nao katika masuala ya maendeleo na diplomasia.
Kauli hiyo imekuja baada ya Jumuiya ya Madola kutoa wito kwa Tanzania kuchukua hatua kuhusu masuala yanayohusu utawala wa sheria na haki za kisiasa, ikiwemo suala la Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, ambaye amekuwa akishikiliwa gerezani kwa tuhuma za uhaini tangu Aprili 2025.
Jumuiya hiyo imetoa muda wa siku 30 kwa Tanzania kushughulikia suala hilo, hatua iliyozua mjadala kuhusu mipaka kati ya ushirikiano wa kimataifa na mamlaka ya ndani ya nchi.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikisisitiza kuwa taasisi zake za kisheria zinafanya kazi kwa uhuru na kwamba masuala yanayohusu kesi mahakamani yanapaswa kuachwa kupitia taratibu za kisheria.
Kwa upande mwingine, vyama vya upinzani na baadhi ya mashirika ya haki za binadamu vimekuwa vikitoa wito wa kuhakikisha kuwa haki za msingi za kisiasa na taratibu za kisheria zinafuatwa katika kushughulikia kesi zenye uzito wa kisiasa.