Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Seyed Abbas Araghchi, amewasilisha ujumbe maalum kwa Katibu Mkuu wa Hezbollah, Sheikh Naim Qassem, akisisitiza msimamo thabiti wa Tehran wa kuendelea kuliunga mkono kundi hilo na msisitizo wa kusitisha vita nchini Lebanon.

Katika ujumbe huo, Waziri Araghchi amebainisha kuwa Iran itaendelea kutoa ushirikiano na kuunga mkono vuguvugu la kutafuta haki na uhuru, hususan Hezbollah. Ameeleza kuwa msimamo huo ni muendelezo wa ahadi ya kihistoria iliyoachwa na Imamu shahidi na ni utekelezaji wa agano kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Grand Ayatollah Seyed Ali Khamenei.

Kuhusu masuala ya kidiplomasia, taarifa hiyo imeweka wazi sharti kuu la Iran katika mchakato wowote wa amani. Imesisitizwa kuwa, tangu mwanzo wa majadiliano, Iran imesimama kidete kuwa makubaliano yoyote yanayohusisha Marekani lazima yaende sambamba na usitishaji vita nchini Lebanon. Hoja hii imeelezwa kuendelea kuwa kipaumbele na takwa la msingi la Serikali ya Jamhuri ya Kiislamu na wananchi wake.

Aidha, ujumbe huo umefichua taarifa kuhusu juhudi za hivi karibuni za kidiplomasia. Imebainishwa kuwa katika pendekezo la hivi punde lililotolewa na Iran kupitia kwa wasuluhishi wa Pakistan, ambalo linalenga kusitisha vita kwa kudumu, suala la kuijumuisha Lebanon katika makubaliano ya kusitisha mapigano limesisitizwa kwa uzito mkubwa.

Ujumbe huu wa kidiplomasia unathibitisha wazi msimamo wa Iran kuhusu mshirika wake mkuu nchini Lebanon, Hezbollah, na unaashiria kuwa Tehran inaichukulia Lebanon kama kipengele kisichoweza kutenganishwa katika kutafuta suluhu ya kudumu ya usalama na amani katika ukanda huo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *