PARIS – Serikali ya Ufaransa imempiga marufuku Waziri wa Usalama wa Taifa wa Israel, Itamar Ben-Gvir, kuingia katika ardhi ya taifa hilo, kufuatia kile kilichotajwa kuwa ni mienendo isiyokubalika dhidi ya raia wa Ufaransa na Ulaya.

Akithibitisha hatua hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ufaransa, Jean-Noël Barrot amesema: “Kuanzia leo, Itamar Ben-Gvir amepigwa marufuku kuingia katika ardhi ya Ufaransa. Uamuzi huu unafuatia vitendo vyake viovu dhidi ya raia wa Ufaransa na Ulaya waliokuwa abiria kwenye msafara wa meli za Global Sumud Flotilla.”Waziri Barrot alisisitiza msimamo wa nchi yake akisema kuwa, Ufaransa haiwezi kuvumilia kuona raia wake wakitishiwa au kufanyiwa ukatili wa namna hiyo, hasa ikifanywa na afisa wa umma.

Alibainisha kuwa vitendo hivyo ni muendelezo wa mfululizo wa kauli na matendo ya kushtusha, ikiwemo uchochezi wa chuki na ghasia dhidi ya Wapalestina. Aidha, ameeleza kuwa akishirikiana na mwenzake wa Italia, wameuomba Umoja wa Ulaya (EU) kumwekea vikwazo waziri huyo.

Hatua hii kali inakuja muda mfupi baada ya Ben-Gvir kuchapisha video mtandaoni ikimuonyesha akiwadhihaki wanaharakati wa Gaza waliokamatwa na vikosi vya Israel. Katika video hiyo, wanaharakati hao walionekana wakiwa wamefungwa vitambaa machoni, wamepiga magoti na kufungwa mikono yao katika Bandari ya Ashdod.

Tukio hilo limeibua shutuma kali kimataifa, kiasi cha kumfanya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, kukaririwa akisema kuwa mwenendo wa Ben-Gvir “hauendani na maadili na kanuni za Israel.”Kufuatia uamuzi huu, Ufaransa inakuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kuchukua hatua kwa vitendo, huku wimbi la shinikizo la kidiplomasia likizidi kusambaa.

Waziri Mkuu wa Uhispania tayari ametangaza kuanzisha juhudi za kuwapiga marufuku mawaziri wa Israel kuingia ndani ya nchi za Umoja wa Ulaya (EU), na Italia inashinikiza vikwazo vya pamoja vya EU. Aidha, imeripotiwa kuwa Croatia imegoma kumpokea balozi wa Israel kwa takriban miezi saba sasa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *