Katika mashambulizi makali yaliyoshuhudiwa usiku wa leo, picha na mikanda ya video iliyotolewa inathibitisha kuwa Urusi imetumia kombora la balestiki aina ya ‘Oreshnik’ nchini Ukraine. Hatua hii inakuja na kuthibitisha maonyo yaliyokuwa yametolewa na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, ambaye alitegemea ripoti za siri za kijasusi kutoka Marekani na shirika la NATO.
Kulingana na taarifa, mashambulizi hayo ya usiku wa leo hayakuhusisha tu kombora hilo la Oreshnik, bali pia yaliambatana na makombora mengine na makundi ya droni za kujitoa mhanga.
Mfumo huu wa makombora wa Oreshnik uliingizwa kwenye uwanja wa vita kwa mara ya kwanza mnamo Novemba 21, 2024, wakati wa operesheni ya kijeshi ya Urusi nchini Ukraine, na umekuwa ukivutia hisia za wataalam wa masuala ya kijeshi ulimwenguni.
Tahadhari kubwa inatokana na uwezo wake wa kipekee unaojumuisha mwendo kasi wa haipasoniki (hypersonic), muundo wa hatua nyingi (multi-stage), na matumizi ya teknolojia ya MIRV (Multiple Independently Targetable Reentry Vehicle). Jambo linaloshangaza wengi ni kwamba, teknolojia hii tata imeambatanishwa kwenye kombora ambalo si la nyuklia, hali ambayo hapo awali ilizoeleka kuonekana tu kwenye makombora ya kimkakati ya nyuklia ya masafa marefu (ICBM).
Wachambuzi wa masuala ya kiusalama wanaeleza kuwa, kupelekwa kwa kombora la Oreshnik kunatafsiriwa kama ufafanuzi mpya na wa wazi wa msimamo wa kijeshi wa Urusi. Inatazamwa kama mbinu ya kutoa ujumbe na kuweka kizuizi mbele ya nchi wanachama wa NATO, hususan washirika wake wa barani Ulaya.