Rais wa Marekani, Donald Trump, ametangaza rasmi kujiuzulu kwa Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa, Tulsi Gabbard, hatua inayotajwa kulenga kutoa kipaumbele kwa matibabu ya mume wake, Abraham Williams.

Katika taarifa iliyotolewa na Ikulu ya White House, Rais Trump amethibitisha kuwa Gabbard ataondoka rasmi katika utumishi wa serikali ifikapo tarehe 30 Juni, baada ya kufanya kazi ya “kipekee na ya ajabu.” Uamuzi huo umefuatia mazungumzo kati ya wawili hao katika Ofisi ya Oval (Oval Office) mapema leo.

Rais Trump amebainisha kuwa sababu ya kuondoka kwa Gabbard ni hitaji la kuwa kando ya mume wake, ambaye amegundulika hivi karibuni kuwa na aina adimu sana ya saratani ya mifupa. Rais ameelezea kuguswa kwake na hali hiyo, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa Gabbard wa kuweka kando majukumu ya kitaifa ili kupambana na vita hiyo ya kiafya pamoja na mumewe ni uamuzi wa haki na wa kupongezwa.

“Tulsi amefanya kazi ya ajabu, na tutamkosa. Sina shaka kwamba Abraham atarejea katika hali yake njema hivi karibuni,” ilisema taarifa ya Rais.

Kufuatia kuondoka huko, Rais Trump amemteua Aaron Lukas, ambaye kwa sasa ni Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Ujasusi wa Kitaifa, kuwa Kaimu Mkurugenzi wa idara hiyo. Lukas, ambaye anatambulika kwa uzoefu na heshima kubwa ndani ya sekta ya ujasusi, anatazamiwa kuendeleza majukumu ya ofisi hiyo bila kuwepo kwa mkwamo wowote wa kiusalama.

Hadi sasa, serikali haijatoa ufafanuzi zaidi kuhusu mchakato wa kumpata mrithi wa kudumu wa nafasi hiyo, huku macho ya wengi yakiwaelekea familia ya Gabbard katika kipindi hiki kigumu cha mapambano ya kiafya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *