Poland imepiga hatua kubwa katika kuimarisha ulinzi wake wa anga baada ya kuthibitisha kuwasili kwa ndege tatu za kwanza za kivita aina ya Lockheed Martin F-35 Lightning II zilizotengenezwa nchini Marekani. Ndege hizo zimetua rasmi katika Kambi ya Jeshi la Anga ya Łask, ikiwa ni sehemu ya mpango kabambe wa usambazaji wa ndege hizo utakaokamilika ifikapo mwaka 2029.

Ujio wa ndege hizi ni mwendelezo wa mkataba mkubwa uliotiwa saini mwaka 2020 wakati wa muhula wa kwanza wa Rais Donald Trump. Katika mkataba huo wenye thamani ya dola bilioni 4.6, serikali ya Warsaw ilifanya oda ya jumla ya ndege 32 za kisasa aina ya F-35A.

Taarifa kutoka jeshi la Poland zinasema kuwa marubani wa taifa hilo tayari wako nchini Marekani wakiendelea na mafunzo maalum ili kujiandaa kikamilifu kuendesha mashine hizo za vita zenye teknolojia ya hali ya juu.

Hii inatazamwa kama hatua muhimu ya kuongeza nguvu ya kijeshi ya Poland na kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi baina ya Warsaw na Washington.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *