Ripoti mpya kutoka gazeti la The Wall Street Journal (WSJ) imebainisha kuwa nchi za Uchina na Urusi zimeongeza kwa kiasi kikubwa operesheni zao za kijasusi nchini Cuba katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni.

Kulingana na maafisa wa usalama, idadi ya wafanyakazi wa mataifa hayo wawili katika vituo vya ufuatiliaji wa kielektroniki nchini Cuba imeongezeka mara tatu tangu mwaka 2023. Hatua hii inaelezwa kuwa na lengo mahususi la kufuatilia mienendo ya kijeshi ya Marekani katika jimbo la Florida.

Takwimu zinaonyesha kuwa, kati ya vituo 18 vya mawasiliano ya kijasusi (signals intelligence) vilivyopo nchini humo, Uchina inaendesha vituo vitatu huku Urusi ikiendesha viwili. Baadhi ya vituo hivyo vinasemekana kuendeshwa kwa ushirikiano wa karibu na serikali ya Cuba.

Uchunguzi unaonyesha kuwa vituo hivyo vinalenga kufuatilia Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) iliyoko Tampa, na Kamandi ya Kusini (SOUTHCOM) inayopatikana karibu na mji wa Miami. Hata hivyo, maafisa wamebainisha kuwa mawasiliano mengi yanayonaswa na vituo hivyo ni yale yasiyo na hadhi ya siri.

Afisa mwandamizi wa serikali ya Marekani amevitaja vituo hivi vilivyopo Cuba kuwa miongoni mwa machapio muhimu zaidi ya ujasusi ya Beijing na Moscow nje ya mipaka yao, huku kukiwa na hofu kuwa upanuzi zaidi unaweza kufanyika siku za usoni.

Kufuatia uvumbuzi huo, utawala wa Rais Trump umeanza kuchukua hatua madhubuti za kuongeza shinikizo dhidi ya Cuba. Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha ufuatiliaji wa angani kupitia safari za ndege zisizo na rubani (drones) zinazofanyika karibu kila siku, pamoja na kuelekeza upya setilaiti za kijasusi ili kukabiliana na tishio hilo linaloendelea kukua.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *