Katika hatua inayoangazia mgawanyiko wa kiserikali, Amaryllis Fox Kennedy, ambaye ni mkwe wa Robert F. Kennedy Jr. na mshirika wa karibu zaidi wa Tulsi Gabbard katika idara ya ujasusi, amejiuzulu nyadhifa mbili kuu kufuatia kutokubaliana kwake na vita vya Rais Trump dhidi ya Iran.

Kennedy anatarajiwa kuachia ngazi wiki hii kama Naibu wa Gabbard katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa (ODNI), pamoja na wadhifa wake wa Mkurugenzi Mshiriki katika Ofisi ya Usimamizi na Bajeti (OMB), ambapo alikuwa na jukumu la kusimamia bajeti za siri za ujasusi.

Licha ya kujiuzulu huko, taarifa zinaeleza kuwa ataendelea kuhudumu katika wadhifa wake wa tatu kama mjumbe wa Bodi ya Ushauri wa Ujasusi ya Rais (PIAB).Kennedy ana historia ndefu katika masuala ya kiusalama, akiwa amehudumu kama afisa wa siri wa Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kwa muda wa miaka minani, na pia ni mwandishi.

Msimamo wake dhidi ya mzozo na Iran ulifahamika tangu kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2024, ambapo katika mahojiano na Tucker Carlson, aliweka wazi kupinga kwake vita dhidi ya taifa hilo.Duru za kuaminika zimearifu kuwa suala la vita na Iran ndio msukumo mkuu wa uamuzi wake wa kuondoka.

Hata hivyo, katika barua pepe yake ya kujiuzulu, Kennedy hakutaja suala hilo, badala yake alimpongeza Rais Trump na kueleza kuwa anarejea katika “sekta binafsi.”Kujiuzulu kwa Kennedy kunamfanya kuwa afisa wa pili mwandamizi wa ujasusi kuachia ngazi kutokana na mzozo wa Iran.

Mapema mwezi Machi, Joe Kent, aliyekuwa Mkurugenzi wa Kituo cha Kitaifa cha Kukabiliana na Ugaidi, alijiuzulu huku akidai hadharani kwamba Rais Trump alisukumwa kuingia vitani kutokana na “shinikizo kutoka Israel na ushawishi wake mkubwa nchini Marekani.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *