Waraka wa siri wa kidiplomasia wa Pakistan uliotolewa kwa mara ya kwanza tarehe 18 Mei, unathibitisha kuwa mwanadiplomasia mkuu wa Marekani alishinikiza kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Imran Khan, mwaka 2022.
Kwa mujibu wa waraka huo uliodokezwa na mtandao wa Drop Site News, Donald Lu, ambaye kwa wakati huo alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Asia Kusini na Kati, alimwambia Balozi wa Pakistan mjini Washington, Asad Majeed Khan, kwamba “yote yatasamehewa” endapo kiongozi huyo angeondolewa kupitia kura ya kutokuwa na imani naye bungeni.
Mawasiliano hayo ya kidiplomasia yalifanyika baada ya Bw. Khan kufanya ziara mjini Moscow na kukutana na Rais wa Urusi, Vladimir Putin, tarehe 24 Februari 2022, siku ambayo Urusi ilianzisha uvamizi wake nchini Ukraine.
Katika waraka huo wa tarehe 7 Machi 2022 uliowekewa alama ya “Siri / Kutosambazwa,” Bw. Lu ananukuliwa akieleza kuwa mkutano wa Khan na Putin ulizua “wasiwasi mkubwa” kwa serikali ya Washington.
Kwa upande wake, Serikali ya Islamabad ilijitetea ikisema kuwa safari ya Khan nchini Urusi ilikuwa imepangwa miezi kadhaa mapema na haikuwa na uhusiano wowote na uvamizi wa Ukraine, ikisisitiza kuwa Pakistan ilikuwa inafuata sera ya “kutoegemea upande wowote” katika mzozo huo.
Zaidi ya hayo, waraka huo ulijumuisha tathmini ya Balozi Asad Majeed Khan aliyoamini kuwa ujumbe wa Donald Lu ulikuwa umepata baraka kutoka Ikulu ya Marekani (White House).
Balozi huyo pia alibainisha kuwa matamshi ya mwanadiplomasia huyo wa Marekani yalikuwa ni dhahiri kuingilia kati masuala ya ndani ya kisiasa ya Pakistan.